Taifa Stars ya Tanzania leo Machi 28, 2017 saa 10:00 jioni
inaingia tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kucheza na Intamba
Murugamba ya Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, kwa mujibu
wa kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa ya FIFA.
Huu ni mchezo wa pili kwa Taifa Stars kucheza ndani ya wiki moja
baada ya ule wa awali dhidi ya The Zebras ‘Pundamilia’ wa Botswana
uliofanyika Uwanja huo wa Taifa, jijini Dar es Salaam Jumamosi
iliyopita.
Katika mchezo huo wa Jumamosi, Taifa Stars ambayo kwa sasa inanolewa
na Salum Mayanga akisaidiwa na Patrick Mwangata ambao ni makocha wapya
wa kikosi hicho, walishinda kwa mabao 2-0.
Tayari Intamba Murugamba wametua nchini tangu juzi Jumapili saa 4.30
asubuhi na kufikia Hoteli ya De Mag iliyoko, Kinondoni, Dar es Salaam na
jioni yake walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini. jana
Jumatatu, inafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ndani ya kikosi hicho wamo washambuliaji wawili wanaotamba katika
klabu za Simba na Young African za Dar es Salaam. Nyota hao ni Amisi
Tambwe wa Young Africans na Laudit Mavugo wa Simba.
Jana Jumatatu Machi 27, 2017 saa 8.30 alasiri nyota hao wakiongozana
na kocha wao watazungumza na wanahabari namna walivyoajiandaa kucheza na
Taifa Stars ambayo pia ina nyota wengi wanaocheza na wachezaji hao wa
Burundi katika klabu za Simba na Young Africans.
Wakati Mavugo ni mshambuluaji, anatarajiwa kuwa na wakati mgumu mbele
ya walinzi mahiri ambao pia wako Simba kama vile Abdi Banda na Mohammed
Hussein wakati Andrew Vicent anayetoka Young African atakuwa kisiki kwa
Tambwe wanayecheza naye timu moja kama makocha watawapanga.
Kwa upande wake, Mayanga alifurahishwa na ushindi wa Jumamosi
iliyopita dhidi ya The Zebras ya Botswana na hivyo amehimiza Watanzania
kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho.
Katika kuunga mkono wito wa Kocha Mayanga, TFF imebakiza viingilio
vya mchezo huo kuwa sawa na vile vya Jumamosi iliyopita kwani katika
mzunguko ambao unachukua mashabiki wengi kiingilio kitakuwa ni Sh 3,000.
Kwa upande wa VIP “A” Kiingilio kitakuwa ni Sh 15,000 wakati VIP “B”
na VIP “C” kiingilio kitakuwa ni Sh 10,000. Viingilio hivyo vimelenga
kuwaalika Watanzania wengine kwenda uwanjani.
No comments:
Post a Comment